Thursday 13 March 2014

Maonesho ya Kuadhimisha Siku Mlaji Yafunguliwa Jijini Tanga Leo Machi 13, 2014



Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Mhe.Salum Mohammed Chima,leo, Alhamisi, tarehe 13, 2014, amefungua rasmi maadhimisho ya Kitaifa ya Haki za Mlaji kwa mwaka 2014, katika viwanja vya Polisi Mabawa, jijini Tanga, huku akiyataka Mabaraza yanayojishughulisha na Utetezi wa Mlaji kuhakikisha kuwa yanaongeza utoaji wa elimu kwa wananchi ili waweze kujua haki na wajibu wao na kuweza kujua namna wanavyoweza kuhudumiwa na mabaraza hayo katika kutanzua kero wanazokabiliana nazo wakiwa sokoni. 

Ufunguzi huo uliambatana na mdahalo wa wazi la siku moja lililohusisha wanafunzi zaidi ya 200 kutoka Vyuo na Shule za Sekondari zilizopo Mkoani Tanga. Vyuo vilivohusika katika kongamano hilo ni pamoja na Chuo cha Biashara cha Mtakatifu Joseph na Chuo Kikuu cha Eckenforde. Shule zilizoshiriki ni pamoja na Shule ya Sekondari ya Popatlal, Shule ya Sekondari ya Mikanjuni na Shule ya Sekondari ya Usagara. Majadiliano katika mdahalo huo wa wazi yalijikita zaidi katika huduma zinazodhibitiwa na SUMATRA hususan usafirishaji wa abiria mijini, maarufu kama usafiri wa Daladala, udhibiti wa huduma za mawasiliano ya simu za mkononi, athari za bidhaa bandia, haki za mlaji au mtumiaji na udhibiti wa huduma za majisafi.

Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Haki za Mlaji, yaliyoanza jana katika viwanja vya Tropicana, eneo la Mabawa, jijini Tanga, yameandaliwa na kuratibiwa na Jukwaa la Watumiaji (Tanzania Consumer Forum). Maonesho hayo yatafanyika kwa siku nne katika viwanja hivyo vya Tropicana, Mabawa, kuanzia Machi 12 hadi 15, 2014, siku ambayo ndiyo kilele cha maadhimisho ya Haki za Mlaji.
 
Katika maonesho hayo, wananchi wa Jiji la Tanga wanapata fursa ya kujifunza kuhusu shughuli zinazofanywa na Mabaraza ya Ushauri kwa Walaji wa Huduma zinazodhibitiwa na zisizodhibitiwa na Mamlaka za Udhibiti kwa mashirika ya huduma na miundombinu. Aidha walijifunza shughuli za Tume ya Ushindani.

Tume ya Ushindani na Asasi isiyo ya Kiserikali ya “Sauti ya Mtumiaji” ni taasisi mbioi zisizo wadhibiti zilizoshiriki katika maonesho hayo. Washiriki kutoka kwa Mamlaka za Udhibiti ni pamoja na Mabaraza ya Ushauri kwa Walaji wa Huduma zinazodhibitiwa na SUMATRA, EWURA na TCRA. Aidha, Baraza la Ushauri kwa Walaji wa Huduma zinazosimamiwa na TCAA pia lilishiriki katika maonesho hayo.  

Kaulimbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka 2014 inasema “Haki za Mtumiaji wa Simu Zilindwe”. Kaulimbiu hii inalenga kukumbusha mamlaka husika na kampuni za simu kuhakikisha kuwa zinazingatia haki za walaji au watumiaji wa huduma za simu kwa kuondoa kero na kuwezesha matumizi hayo kuwa ya tija zaidi.

Katika banda la Tume la Ushindani,  wananchi waliweza kujifunza kuhusu Haki na Wajibu wa Mlaji, Jinsi ya Kutambua Bidhaa Bandia na namna Tume hiyo inavyoendesha shughuli zake kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment