Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa
ya Haki za Mlaji Kitaifa yamefikia kilele leo kwa maandamano ya wakazi wa Jiji la Tanga, burudani na hotuba
zilizotolewa katika viwanja vya Tropikana Mabawa, Jijini Tanga.
Kilele cha maadhimisho hayo
kilitanguliwa na maandamano ya wakazi wa jiji la Tanga walioongozwa na Bendi ya
Muziki wa Ala (Brass Band) na kuwahusisha wanafunzi wa Shule za Sekondari za
Mikanjuni, Popatlal na Usagara pamoja na Chuo Kikuu cha Eckenforde.
Maandamano hayo yaliyoanzia
katika viwanja vya Uhuru Park majira ya saa nne asubuhi, yalipokelewa na Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Mhe.
Halima Dendegu majira ya saa tano asubuhi. Mhe. Dendegu ndiye aliyekuwa mgeni rasmi katika kilele cha
maadhimisho hayo.
Akihutubia katika kilele cha
maadhimisho hayo, Mhe. Dendegu alizitaka kampuni za simu kupitia na kurekebisha
taratibu na kanuni zao za utendaji ili kuhakikisha kuwa wanazitambua na
kuzilinda haki za watumiaji wa simu ili kuwezesha matumizi ya huduma ya
mawasiliano ya simu kuwa ya tija. Alisema bils kuzingatia haki za watumiaji wa
simu, ni vigumu kupatikana kwa matumizi yenye tija, jambo linaloweza kuathiri
ukuaji endelevu wa sekta hiyo nchini.
Aidha, Mhe. Dendegu aliwataka
watumiaji wa simu kubadilisha miondoko na mienendo ya kutumia simu kwa lengo la
kuwezesha matumizi mazuri kuzingatiwa ili matumizi hayo yaweze kuwa na tija.
Pamoja na kutoa rai kuhusu
matumizi ya simu, Mhe. Dendegu pia aliwataka wananchi kuwa makini wanapokwenda
kufanya manunuzi yao sokoni kwa kuhakikisha kuwa wanatimiza wajibu wao kwa
kukagua na bidhaa wanazotaka kununua badala ya kuzikimbilia kutokana na urahisi
wa bei.
Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa
ya Haki za Mlaji kwa mwaka 2014 Kitaifa yamebebwa na Kaulimbiu isemayo “Haki za
Watumiaji wa Simu Zilindwe”. Kauli mbiu hiyo inalenga kuzitaka Kampuni za Simu
kubainisha Haki za Msingi za Watumiaji wa Huduma za Simu na kisha kuweka
utaratibu wa kuzilinda haki hizo, hasa ikizingatiwa kuwa maendeleo ya Sayansi
na Teknolojia pamoja na Utandawazi, vimesababisha matumizi ya simu hususan za
mkononi kuwa makubwa sana ambapo inakadiriwa kuwa zaidi ya watu bilio tano
ulimwenguni kote wanatumia huduma ya simu za mkononi.
No comments:
Post a Comment