Vyombo vya Udhibiti, Mahakama, Wafanyabiashara Timizeni Wajibu
Wenu-Mulongo
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe.
Magesa Mulongo amevitaka vyombo vya usimamizi wa uchumi na udhibiti wa biashara
na huduma pamoja na wafanyabiashara kwa ujumla kutimiza wajibu wao ili kuhakikisha
kuwa ukiukaji wowote wa sheria za nchi unaowaumiza walaji ambao ni wananchi wa
Tanzania, hauachwi bila wahusika kuchukuliwa hatua stahiki kwa mujibu wa Sheria
za nchi
Mhe. Mulongo alitoa wito huo
wakati akifungua Semina ya siku moja kwa wadau wa Sheria ya Ushindani, Utetezi
wa Mlaji na Udhibiti wa Bidhaa bandia, iliyoandaliwa na Tume ya Ushindani na
kufanyika katika Hoteli ya Kibo Palace, jijini Arusha.
Mhe. Mulongo alisema kuwa
kumekuwa na malalamiko mahali pengi kutokana na utendaji usioridhisha wa vyombo
mbalimbali vya udhibiti na usimamizi wa utendaji wa mfumo wa uchumi wa soko na
kuitaka Tume ya Ushindani kuusoma mfumo mzima wauzalishaji na usambazaji wa
bidhaa bandia na kuchukua hatua kabla ya bidhaa hizo hazijaingizwa sokoni kwa
kuwa mfumo huo utakapodhibitiwa vema, itakuwa vigumu kwa wafanyabishara wasio
waaminifu kuweza kuuza bidhaa hizo sokoni.
Aidha alivitaka vyombo hivyo
kufanya kazi kwa pamoja badala ya kila kimoja kufanya kazi kivyake kwa kuwa
utendaji wa pamoja utawezesha kila chombo kutoa mchango wake stahiki katika kudhibiti
mienendo potofu na kandamizi katika uchumi kwa kuwa wafanyabiahara wasio
waaminifu watatambua mamlaka ya Serikali na vyombo vyake katika kusimamia na
kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Alibainisha kuwa yamekuwepo
malalamiko ya utendaji kwa baadhi ya vyombo vya udhibiti vya Serikali pamoja na
mahakama, na kuwa mashauri yameonekana kutoshughulikiwa kwa weledi na hivyo
kusababisha wahalifu kuachiwa kwa sababu
zinazowavunja moyo wananchi na kusababisha kutoviamini vyombo vya Serikali
vinavyotoa haki katika kutimiza majukumu yao.
Mada mbalimbali ziliwasilishwa
katika Semina hiyo ikiwa ni pamoja na Dhana na Maudhui ya Sheria ya Ushindani, Muundo
wa Sheria ya Ushindani, Utetezi wa Mlaji na Mapambano Dhidi ya Bidhaa Bandia.
Wadau walijadili masuala
mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupendekeza kuifanyia marekebisho sheria ya alama
za bidhaa ili wahalifu wanaojihusisha na biashara za bidhaa bandia zenye
madhara kwa binadamu washitakiwe kwa “kusudio la kufanya mauaji”. Aidha,
wajumbe wengine walielezea umuhimu wa elimu ya utetezi wa mlaji kusambazwa kuanzia
ngazi za shule za msingi ili jamii ijayo ya Watanzania ikue ikiwa na uelewa
mzuri zaidi wa masuala ya msingi ya haki na wajibu wa mlaji na kuwa tayari
kutetea haki zake na kufhamu wajib wake awapo sokoni.
Aidha, Chama cha Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA) Mkoa, walitangaza azma ya kuratibu mchakato wa kuanzisha Chama cha Walaji Mkoani Arusha na kuwataka washiriki wa Semina kujitokeza kuwa wanachama waasisi wa chama hicho.
Semina hiyo ilihudhuriwa na wadau
mbalimbali wakiwemo wawakilishi wa Jeshi la Polisi, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu
wa Serikali, Mawakili wa Kujitegemea, wawakliishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA), Idara ya Maliasili, Maafisa Biashara na Ushirika wa Mikoa, Wilaya na
JIji, Wawaklishi wa Taasisi za Wafanyabiashara, Wafanyabiashara na wazalishaji
na waandishi wa habari.
No comments:
Post a Comment