Tuesday 15 April 2014

Naibu Waziri wa Viwanda Atembelea FCC na Kuitaka Ifungue Matawi ya Kanda



Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Nchini, Mhe. Janeth Mbene (MB) leo alitembelea Tume ya Ushindani ambapo aliitaka Tume hiyo kufungua ofisi za Kanda ili kuweza kuongeza juhudi za kutoa elimu ya mlaji kwa wananchi walio wengi sehemu mbalimbali nchini.

Mhe. Mbene alitoa wito huo baada ya Kupata fursa ya kujifunza kwa vitendo jinsi ya kutofautisha bidhaa bandia na halisi ambapo sampuli zake zilikuwepo katikaukumbi wa mikutano wa Tume hiyo, Ubungo Plaza, jijini Dar es Salaam.

Alisema “Wananchi wengi wa Tanzania tuna tatizo la kupenda kuamini kila tunaloambiwa na wafanyabiashara, hivyo ni vema Tume ikafungua ofisi walau za kanda ili iweze kuongeza kupeleka elimu hii kwa wananchi waweze kuelewa kuwa zipo bidhaa bandia na kuna mienendo potofu katika soko ili waweze kuwa makini zaidi.

Alidha, Mhe. Mbene aliitaka Menejimenti ya Tume kuwasilisha maelezo kuhusu kuongezewa bajeti ili kuwezesha utendaji wenye ufanisi wa chombo hicho ambacho kina wajibu wa kusimamia utendaji wa uchumi wa soko.

Waziri Mbene pia alipokea maoni ya Tume ya Ushindani kuhusu umuhimu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuanzisha Sheria za kusimamia na kudhibiti kusambaa kwa bidhaa bandia ambapo ilibainika kuwa kuna kiasi kikubwa cha bidhaa zinazoshukiwa kuwa ama ni bandia au zipo chini ya kiwango zinazoingizwa Tanzania bara kutoka Tanzania Vsiwani kwa njia za magendo.

Aliitaka Tume ya Ushindani kuwasilisha mapendekezo yake kwake ili aweze kuona namna bora ya kuwasilisha ushauri huo Seikalini.

Waziri Mbene pia aliitaka Tume ifanye kazi kwa kushirikiana kwa karibu na vyombo vinavyofanya shughuli zinazoshabihiana nazo akibainisha Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) ambazo pia zinafanya kazi za kumlinda mlaji.

Katika ziara hiyo Waziri Mbene aliambatana na Mkurugenzi Msaidizi wa Sera na Mipango-Bajeti, Bibi Elizabeth Msengi, Afisa Habari, Edward Nkomola na Katibu wake, Athumani Nkhungu. 

Akimaribisha Waziri Mbene katika Tume Mkurugenzi Mkuu wa Tume hiyo, Dk. Frederick Ringo alielezea kuwa shughuli za Tume hiyo zinashindwa kukamilika kwa ufanisi kutokana na ufinyu wa bajeti na kuelezea umuhimu wa Serikali kuipatia Tume hiyo fungu la kutosha la bajeti ya utendaji wa shughuli zake.

Kabla ya ukaribisho wa Dk. Ringo kwa Naibu Waziri, Mkuu wa Idara ya Utetezi wa Mlaji, Martha Kisyombe, alielezea kwa kifupi shughuli za idara hiyo huku akibainisha changamoto inayowakabili ya namna ya kutatua kero za mlaji kwa kutumia njia ya mahakama. Bi. Kisyombe alisema kuwa katika mapendekezo ya marekebisho ya Sheria, Tume ya Ushindani inatarajia kutumia mbinu za Taratibu Mbadala za Utanzuajij wa Migogoro baina ya walaji na wafanyabiashara (Alternative Dispute Resolution -ADR) ili kuharakisha utanziaji wa migogoro hiyo na kupunguza muda mwingi wanaopoteza wamaji katika kutanzua mashauri madogo madogo katika mahakama za kawaida.

Aidha, Mkuu wa Idara ya Udhibiti wa Bidhaa Bandia, John Mponela, alieleza kuwa Tume imeendelea kufanya kaguzi mbalimbali katika maingilio makuu ya bidhaa nchini (Bandar ya Dar es Salaam na Vitengo Mahsusi vya Makontena), pamoja na madukani na mikoani kubaini na kukamata bidhaa bandia zinazoingizwa nchini kinyume cha Sheria ya Alama za Bidhaa ya mwaka 1963, iliyorekebishwa.

Alieleza kuwa kwa sasa Tume inakabiliwa na changamoto kubwa ya kukosekana kwa Sheria ya Udhibiti wa Bidhaa Bandia katika Tanzania Visiwani, jambo ambalo limesabaisha shehena kubwa ya bidhaa zinzohofiwa kuwa ni bandia kuingizwa Tanzania bara kwa njia zisizo rasmi ambapo hazilipiwi ushuru stahiki na zinasababisha ushindani katika soko kutokuwa katika mizania sawa.

No comments:

Post a Comment