Tuesday 29 August 2017

FCC Zapata Kaimu Mkurugenzi Mkuu Mpya, Dk. John Kedi Mduma

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Prof. Mkenda Amtambulisha Kaimu Mkurugenzi Mkuu Mpya, Dk. John Mduma Kwa Wafanyakazi wa FCC
Awataka Wafanyakazi Kuendelea Kufanya Kazi Nzuri kwa Weledi na Uadilifu Zaidi

Dar es Salaam, Agosti 29, 2017. Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji  (Biashara), Prof. Adolph Mkenda, amemtambulisha Kaimu Mkurugenzi Mkuu Mpya wa Tume ya Ushindani (FCC), Dk. John Kedi Mduma, katika Mkutano Maalum na Menejimenti na wafanyakazi hao uliofanyika mchana katika ukumbi wa Mikutano wa FCC, Jengo la GEPF House, Agosti, 28, 2017.

Akizungumza katika kikao cha utambulisho huo, Prof. Mkenda alisema kuwa anafahamu kuwa kazi ya Tume ni ngumu na muhimu sana kwa uchumi wa taifa na hivyo akawataka wafanyakazi kuendelea kufanya kazi nzuri wanayoifanya kwa weledi na kwa uadilifu zaidi ili kutunza heshima ya Serikali na Taasisi na kuhakikisha kuwa azma ya Serikali ya Kuwa na Uchumi wa Viwanda inafanikiwa.

Alisema kuwa Serikali haitakubali kuona kuwa wafanyabiashara wasio waaminifu wanaingiza na kuuza bidhaa bandia bila kuchukuliwa hatua stahiki kwa kuwa bidhaa hizo ambazo mara nyingi huwa chini ya kiwango na huuzwa kwa bei chee, husababisha wazalishaji wa bidhaa halisi na zinazokidhi viwango kusita kufungua viwanda hapa nchini kwa kuwa hawataweza kushindana na bidhaa bandia zinazoharibu sökö.

“Serikali ipo pamoja nanyi, tutawalinda na kuwatetea, chapeni kazi, misogope na msikate tamaa na msimamie kwenye sheria. Isipokuwa sasa mnatakiwa kufanya kazi zenu kwa uadilifu na weledi zaidi ili taswira nzuri ya taasisi iendelee kulindwa”, alisisitiza Prof. Mkenda. Aliwataka wafanyakazi kumpa ushirikiano mkubwa Kaimu Mkurugenzi MkuuDk. John Mduma, katika kuhakikisha kuwa taasisi inapiga hatua zaidi katika kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria.

Prof. Mkenda aliwapongeza wafanyakazi wa FCC kwa kufanya kazi nzuri kwa weledi na uadilifu katika mazingira magumu ya uhaba wa rasilimali na vitendea kazi na kuelezea kuwa Serikali itaendelea kuwaunga mkono na kuboresha maslahi yao kadiri hali itakavyoruhusu.

“Madhali mnaongeza uchapaji kazi na maslahi yanakwenda kuwa mazuri zaidi na madhali kazi yenu inakwenda kuwa muhimu kuliko wakati wote, mtaangaliwa zaidi kuliko wakati wowote ili kubaini nani anakwamisha juhudi za Serikali. Kwa hiyo wakati mnafanya kazi nzuri, asitokee mmoja kati yenu atakayeharibu sifa yenu nzuri,” alisisitiza Prof. Mkenda.

“Serikali haitawaingilia katika maamuzi yenu ya kimahakama bali patakapokuwa na maswali tutawauliza na msichoke kutujibu ili tuweze kuelewa ukweli ulivyo. Kazi yenu ni ngumu na inasababisha mpigwe majungu na kusingiziwa mambo mbali mbali, hivyo tunalazimika kuuliza. Muilinde taswira ya taasisi yenu kwa kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na weledi kama mnavyolinda mboni ya jicho,” aliasa Prof. Mkenda na kuongeza kuwa kamwe Serikali haitavumilia kampuni zinazotaka kuimairisha ukiritimba (Monopoly) katika soko kwa kuwa zinawakandamiza walaji wa bidhaa na huduma na kuua ushindani katika soko na hivyo akawataka watendaji wa Tume kuendelea kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria lakini waepuke pia kutumia lugha za kibabe na kuwaasa wawasaidie wafanyabiashara (hususan kuhus suala la kuingiza bidhaa bandia) kwa lugha wezeshi ili wasitumbukie tena kwenye hatari ya kuagiza bidhaa bandia na kukamatwa mara kwa mara.

Kabla ya kumtambulisha Dk. Mduma, Prof. Mkenda alimpongeza Dk. Frederick Shadrack Ringo kwa kuiendesha Taasisi hiyo kwa weledi kwa kipindi cha muhula wake wa miaka minne na kumtakia kila la kheri baada ya kuhitimisha muhula wa uongozi wake FCC.

Aidha, Dk. Frederick Ringo aliezea shukrani zake kwa imani ambayo Serikali ilimpa katika kuiongoza Tume ya Ushindani pamoja na ushirikiano alioupata kutoka kwa wafanyakazi wa Tume na viongozi wa Serikali. Alisema kutoka na na ushirikiano huo  FCC imeweza kupiga hatua zaidi kuliko alivyoikuta. Aidha, alimweleza Katibu Mkuu kuwa kuwa kwa sasa taasisi ina upungufu wa wafanyakazi zaidi ya 50 na inahitaji kuwa na ofisi ya kudumu pamoja na ghala za kuhifadhi bidhaa bandia zinazosubiri kukamilika kwa hatua za kisheria kabla ya kuteketezwa.

Akizungumza baada ya kutambulishwa kwa wafanyakazi, Dk. John Mduma alielezea kufurahishwa kwake na mapokezi mazuri aliyoyapata lakini akabainisha kuwa ataelezea viapumbele vyake wakati atakapozungumza na wafanyakazi baada ya kukabidhiwa rasmi ofisi mapema hivi karibuni.

Dk. John Kedi Mduma, ambaye ni Mchumi na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ameteuliwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Charles Mwijage (MB) kushika wadhifa huo kuanzia tarehe 28 Agosti, 2017 baada ya muhula wa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo, Dk. Frederick Shadrack Ringo (Wakili) kuisha Agosti 1, 2017. Prof. Mkenda alisema kuwa Dr. Mduma ameteuliwa kushika wadhifa huo kwa kipindi cha mpito wakati ambapo taratibu za uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu mpya zikiendelea kukamilishwa kwa mujibu wa Sheria ya Ushindani Na. 8 ya mwaka 2003.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasilaino na Mahusiano ya Umma, Tume ya Ushindani, Dar es Salaam.

Kwa Maelezo zaidi wasiliana na Frank S. Mdimi. Afisa Mwandamizi, Mawasiliano na Mahusiano ya Umma, Tume ya Ushindani, Simu ya Mkononi +255784762437, Barua Pepe fmdimi@competition.or.tz


No comments:

Post a Comment