NOTISI YA TUME YA USHINDANI KWA
WAFANYABIASHARA NCHINI TANZANIA
(Imetolewa
chini ya Kifungu Na. 9(1)(b) cha Sheria ya
Ushindani, 2003)
Sheria ya Ushindani, Namba 8 ya Mwaka
2003 imetungwa kwa ajili ya kulinda na kushajiisha ushindani wa dhati katika mfumo
wa uchumi wa soko na kumlinda mlaji/mteja dhidi ya mbinu na mienendo potofu na
onevu ya kibiashara.
Ili kusimamia kwa ufanisi misingi ya
ushindani katika uchumi wa soko na kuhakikisha kuwa mlaji/mteja analindwa
ipasavyo, Sheria hii imekataza mambo kadhaa ambayo yamegawanywa katika mafungu makubwa matatu ambayo ni:
a) Makubaliano yanayokiuka ushindani
(Anti-competitive agreements) (Vifungu vya 8 na 9).
b) Matumizi mabaya ya nguvu ya soko
(Misuse of Market Power) (kifungu cha 10).
c) Miungano ya Kampuni inayoimarisha
hodhi ya soko (Mergers and Acquisitions, Kifungu cha 11).
Hivi karibuni, ilisikika katika
vyombo vya habari kuwa wafanyabiashara sehemu mbalimbali nchini, bila ya
kuwajali walaji/wateja wao, waliamua kufanya mgomo na kufunga biashara zao kwa sababu ya
kulalamikia utumiaji wa mashine za kielektroniki za kutoa risiti kwa mteja
(EFD), jambo lisilowahusu wateja wao. Mgomo huo ulileta usumbufu na kuwaumiza zaidi walaji/wateja
kwani hawakuweza kupata bidhaa na huduma walizohitaji kwa wakati na wengine kupata
hasara.
Kwa mujibu wa taarifa za habari,
vitendo vya namna hii vya wafanyabiashara vinaendelea kushamiri siku hadi siku
na wanasahau kuwa Sheria ya Ushindani inazuia vitendo kama hivyo. Sheria ya Ushindani katika kipengele
cha 9(1)(b) inazuia washindani katika biashara kuingia katika makubaliano ya
kugoma kuuza bidhaa au huduma kwa sababu kitendo hicho husababisha mlaji
(consumer)/mteja (customer) kukosa haki yake ya kisheria ya kupata bidhaa au
huduma muhimu.
Kutokana na ufafanuzi huu hapo juu, Tume
ya Ushindani inatoa notisi hii kwa wafanyabiashara wote nchini kuwa:-
1) Kufanya mgomo wa kuuza bidhaa na
huduma kwa walaji/wateja ni
kinyume cha Sheria ya Ushindani, Na. 8/ 2003, na hatua za kisheria zinaweza
kuchukuliwa dhidi yao.
2) Jitihada za kutanzua migogoro ya
kibiashara kati yao na taasisi za Serikali haziwahusu walaji/wateja wao na
kitendo chochote cha kuwaumiza walaji na kuzuia ushindani katika soko ni
kinyume cha Sheria ya Ushindani, Na. 8/ 2003, na hatua za kisheria zinaweza
kuchukuliwa dhidi yao.
POKEA NOTISI HII KUWA Tume ya
Ushindani itafanya uchunguzi wa migomo iwapo itatokea tena kwa mjibu wa Sheria
ya Ushindani, Na. 8/ 2003. Pia tahadhari inatolewa kwa wahusika wote kuwa
makini na vitendo vya kugoma kuuza bidhaa au hudumu ili kuepuka hatua kali za
kisheria kuchukuliwa dhidi yao.
NOTISI HII IMETOLEWA NA TUME YA USHINDANI
TAREHE 19 Septemba, 2014
FREDERICK RINGO
MKURUGENZI MKUU
TUME YA USHINDANI
No comments:
Post a Comment