TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
FCC Yakamata
Simu Bandia za Sh. 72.25m/-
Dar es
Salaam, Septemba 13, 2014. Tume
ya Ushindani imeendesha zoezi la ukaguzi wa kushtukiza katika eneo la Kariakoo
na kukamata simu bandia za mkononi aina ya Samsung na Blackberry.
Zoezi hilo lililofanyika
Septemba 11, 2014 liliwezesha kukamatwa kwa simu bandia 289 zenye jumla ya thamani
ya Sh. 72,250,000.
Uchunguzi zaidi umebaini kuwa
thamani iliyotajwa ya bei ya soko ya simu hizo bandia ni robo tu ya thamani ya
simu halisi, lakini simu hizo bandia zilizokamatwa baadhi zilikutwa zimefungashwa
kwenye maboksi ya simu halisi.
Wamiliki wa Maduka yaliyokaguliwa
na simu bandia kupatikana yanamilikiwa na Hamadi Bakari Hamadi (simu 27),
Hamadi Juma Musa (simu 62 na maboksi matupu 47), Fatuma Gharib Mohammed (simu 72
na betri 5), Jarade Zahor Mohammed (simu 47), Selemani Juman Selemani (simu 35)
na Bakari J. Khatib (simu 44 na simu moja isiyo na nembo iliyokuwa ikifanana na
simu za Samsung pamoja na simu moja bandia
ya Blackberry).
Wafanyabiashara husika wote
walipatiwa hati za kukamatiwa bidhaa zao. Aidha wahusika walitoa maelezo katika
kituo cha polisi cha Msimbazi kuhusiana na na kukamatwa na bidhaa hizo ili
hatua zaidi za kisheria ziweze kuchukuliwa.
Wafanyabiashara husika
wamekwishaagizwa hatua za kuchukua kwa mujibu wa Sheria ya Alama za Bidhaa,
inayokataza biashara ya bidhaa bandia. Kwa mujibu wa Sheria hiyo,
wafanyabishara wanaokamatwa na bidhaa bandia hutakiwa kulipa faini stahiki
pamoja na gharama za uteketezaji wa shehena za bidhaa zilizokamatwa, kulingana
na tathmini inayofanyika kuhusiana na bidhaa hiyo.
Zoezi hilo la ukaguzi wa
kushitukiza lilitokana na maombi ya Wawakilishi wa Hataza na Alama za Biashara
za Samsung, Kampuni ya “Anti Illicit Trade”, yenye makao yake jijini Nairobi,
Kenya.
Ukaguzi wa kushitukiza na
ukamataji wa bidhaa bandia ni zoezi endelevu. Kwa mantiki hiyo, Tume ya
Ushindani inawaasa wafanyabishara wote kujiepusha na kuagiza, kusarifisha,
kuchukua bidhaa hizo toka wakala feki na kujishughulisha na bishara ya bidhaa
bandia kwa kuwa ni kosa la jinai linaloambatana adhabu kali za faini na
kifungo.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya
Ushindani ni Mkaguzi Mkuu wa Sheria ya Alama za Bidhaa mwenye jukumu la
kuongoza mapambano dhidi ya bidhaa bandia katika soko la Tanzania bara. Sheria
inampa mamlaka Mkaguzi Mkuu kufanya ukaguzi wa mizigo na bidhaa katika
maingilio yote ya bidhaa pamoja na maduka, maghala na maeneo yanayomilikiwa na
watu binafsi yanayohofiwa kuficha au kuhodhi bidhaa bandia.
Sheria pia inampa Mkaguzi
Mkuu mamlaka ya kukamata bidhaa zinazoshukiwa kuwa bandia pamoja na kutoa
adhabu za kiutawala ambazo ni pamoja na adhabu za kutoza faini na gharama za
uteketezaji wa bidhaa zilizokamatwa na kuthibitishwa kuwa ni bandia.
Imetolewa leo Septemba 13,
2014 na
Frederick Ringo
MKAGUZI
MKUU, SHERIA YA ALAMA ZA BIDHAA
No comments:
Post a Comment