Friday 18 May 2018

Picha za Semina ya FCC na CHAWASAPI

Mwenyekiti wa CHAWASAPI, Bw. Martin Mbwana (kulia) akipeana mkono na Mgeni Rasmi, Bw. Leo Lyayuka, Mkurugenzi Msaidizi wa Ukuzaji Uwekezaji katika Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, baada ya hotuba ya ufunguzi ya mgeni rasmi, katika ofisi za Tume, Februari 26, 2018. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Utetezi wa Mlaji na Udhibiti wa Bidhaa Bandia, Bi. Magdalena Utouh. 

 Washiriki wa Semina ya FCC na CHAWASAPI iliyofanyiak katika ofisi za Tume Februari 26, 2018 wakiwa katika picha ya pamoja na Mgeni Rasmi, Bw. Leo Lyayuka, Mkurugenzi Msaidizi wa Ukuzaji Uwekezaji katika Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji baada ya ufunguzi wa semina hiyo.

 Mgeni Rasmi katika semina ya CHAWASAPI, Bw. Leo Lyayuka, Mkurugenzi Msaidizi wa Ukuzaji Uwekezaji katika Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, akizungumza na Kaimu Mkurugenzi wa Utetezi wa Mlaji na Udhibiti wa Bidhaa Bandia, Bi. Magdalena Utouh (kushoto) na Msemaji wa CHAWASAPI, Bw. Award Mpandila (kulia) baada ya ufunguzi wa semina hiyo iliyofanyika katika ofisi za Tume, Februari 26, 2018.

  Mwenyekiti wa CHAWASAPI, Bw. Martin Mbwana akizungumza na waandishi wa habari baada ya ufunguzi wa Semina ya FCC na CHAWASAPI iliyofanyika katika ofisi za Tume, Februari 26, 2018.
 
   Mkuu wa Idara ya Udhibiti wa Bidhaa Bandia, Zaytun Kikula, akiwasilisha mada kuhusu udhibiti wa bidhaa bandia wakati wa Semina ya FCC na CHAWASAPI iliyofanyika katika ofisi za Tume, Februari 26, 2018.

    Afisa Mkaguzi wa Bidhaa Bandia na Utetezi wa Mlaji, Diana Augustine, akiwasilisha mada kuhusu Mahitaji na Matakwa, wakati wa Semina ya FCC na CHAWASAPI iliyofanyika katika ofisi za Tume, Februari 26, 2018.

   Mwenyekiti wa CHAWASAPI, Martin Mbwana, akizungumza  wakati wa Semina ya FCC na CHAWASAPI iliyofanyika katika ofisi za Tume, Februari 26, 2018.

    Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Dk. John K. Mduma, akizungumza wakati wa Semina ya FCC na CHAWASAPI iliyofanyika katika ofisi za Tume, Februari 26, 2018.

FCC Yawafanyia Semina Wafanyabiashara wa Pikipiki na Spea Zake

Tume ya Ushindani (FCC) imefanya semina wezeshi kwa wafanyabiashara wa pikipiki na spea zake jijini Dar es Salaam Februari 26, 2018.
 
Semina hiyo iliyohudhuriwa na wawakilishi takriban 30 wakiwemo viongozi wa Chama cha Wafanyabiashara hao, CHAWASAPI, pamoja na wafanyabiashara wa pikipiki na spea zake, ilifunguliwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Ukuzaji Uwekezaji katika Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Bw. Leo Lyayuka.
 
Akifungua semina hiyo alibainisha kuwa jukumu la FCC ni sawa na mwamuzi wa kati katika mpira wa miguu na chombo hicho kimeamua kuwapatia elimu ili kuongezea nguvu eneo la utekelezaji sharia.
 
Mada mbalimbali ziliwasilishwa katika semina hiyo na wafanyabiashara hao kwa ujumla waliishukuru na kuipongeza FCC kwa kuendesha semina hiyo wezeshi. Aidha, waliishauri Tume kuongeza upelekaji wa semina za aina hiyo kwa wafanyabiashara waliopo mikoani ili kuwawezesha wafanyabiashara kuwa wadau muhimu katika ukuaji wa uchumi.
 
 

Wednesday 6 December 2017

Taarifa ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Dk. John Kedi Mduma katika Siku ya Ushindani Duniani Desemba 5, 2017





Hotuba ya Mgeni Rasmi, Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Mhandisi Stella Martin Manyanya (MB) akifungua Maadhimisho ya Siku ya Ushindani Duniani na Semina kwa Wadau wa Sheria ya Ushindani, GEPF House, Dar es Salaam, Desemba 5, 2017

HOTUBA YA MGENI RASMI, NAIBU  WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI, MHESHIMIWA MHANDISI STELLA MARTIN MANYANYA  (MB), KATIKA UFUNGUZI WA  SEMINA KWA WADAU WA SHERIA YA USHINDANI TAREHE 05 DESEMBA, 2017 KATIKA UKUMBI WA MIKUTANO WA GEPF
 
Mwenyekiti wa Tume ya Ushindani -  Prof. Samweli Wangwe,

Makamishna wa Tume ya Ushindani - Mr. Felix Kibodya na Mr. Fadhili  Manongi

Kaimu Mkurugenzi Mkuu Tume ya Ushindani  -Dkt. John Mduma

Menejimenti ya Tume ya Ushindani

Wawakilishi kutoka Wizara, Idara na

Taasisi za Serikali zilizopo hapa,

Viongozi wa Mashirikisho, Vyama na Jumuiya za Wazalishaji na Wafanyabiashara,

Wafanyabiashara mliohudhuria,

Wawezeshaji kutoka Tume ya Ushindani na Taasisi nyingine za Serikali,

Waandishi wa Habari,

Mabibi na Mabwana,

Itifaki Imezingatiwa

 
Habari za asubuhi,

"Awamu ya Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ni ya Uchumi wa Viwanda."

Awali ya yote napenda kuchukua fursa hii adhimu kuwakaribisha washiriki wa kikao kazi hiki kinachojumuisha Mamlaka za Udhibiti, vyama vya wafanyabiashara, wazalishaji na wanahabari.


Leo ni siku ya kipekee ulimwenguni. Ni siku ya Kimataifa ya Ushindani. Siku hii ni muhimu kwetu watendaji wa Serikali na wafanyabiashara pia. Ni siku tunayokumbushana majukumu yetu ya pamoja katika kuendesha uchumi kwa namna inayoleta na kuhakikisha ustawi endelevu katika biashara, uchumi na maslahi ya mlaji ambaye ndiye mteja.

Umuhimu wa kipekee wa siku hii unatokana na ukweli kuwa kwa sasa dunia imekuwa kama kijiji, maendeleo ya Sayansi na Teknolojia yanawezesha taarifa mbalimbali kusafiri kwa haraka kuliko miaka ya nyuma ambapo simu na barua kupitia sanduku la posta ndivyo vilivyokuwa njia kuu za upelekaji taarifa. Kukua kwa teknolojia hizi za upashanaji habari ni matokeo chanya ya kukua kwa ushindani katika sekta ya mawasiliano ulimwenguni.

Kukua kwa ushindani kumewezesha matumizi ya teknolijia za kisasa katika uzalishaji pia, kumeibua njia rahisi za uzalishaji, uuzaji na usambazaji wa bidhaa na huduma yakiwemo matumizi ya biashara mtandao.

Ndugu Wanasemina

Mabadiliko haya ya sayansi, teknolojia na utandawazi, mbali ya kuleta mafanikio yaliyoainishwa, pia yamesababisha changamoto mbalimbali katika soko. Teknolojia imerahisisha kufanyika kwa udanganyifu mkubwa katika soko unaosababishwa na wizi wa milikibunifu na alama za bidhaa ulimwenguni kote. Tanzania pia imekabiliwa na changamoto za bidhaa bandia zinazouzwa kiudanganyifu sokoni.

Ndugu Wanasemina

Sera ya Biashara ya mwaka 2003, imebainisha kuwa Tanzania imeamua kuanzisha mfumo wa kisasa wa usimamizi wa soko kwa kuweka sheria za Ushindani na Udhibiti kwa madhumuni ya kudhibiti kasoro zilizopo katika soko, hasa tabia ya ukiritimba wa soko (kuhodhi soko) ambayo huathiri na kudumaza biashara katika uchumi wa soko.

Uchumi wa soko unahitaji washiriki wengi kuweza kuingia na kufanya shughuli zao bila vikwazo na kuwepo kwa mazingira ya fursa sawa kiushindani (level playing field) ili faida zake ziweze kupatikana. Ni mfumo ambao unaongozwa na nguvu ya uhitaji na ugavi (demand and supply).

Kwa lugha nyepesi kabisa, kama una wauzaji bidhaa kama vipuri au vifaa vya umeme wachache sokoni, watakuwa wanahodhi soko hilo na wanaweza wakala njama kuweka mikakati ya kumnyonya mlaji na kufifisha ushindani baina yao. Mbinu na mikakati hiyo ni pamoja na kupanga bei, kugawana masoko kijiografia, kuficha bidhaa, kutumia vibaya nguvu za soko na kuwaondoa washindani sokoni.

Kukosekana kwa ushindani katika soko, hudumaza tija, ubunifu na ukuaji wa viwanda kwa kusababisha vizuizi vya washindani kuingia sokoni. Kwa upande mwingine, mlaji atakabiliwa na uhaba wa bidhaa.

Ndugu wanasemina

Baada ya Serikali kulegeza masharti ya biashara, kumeibuka wimbi la wafanyabiashara wasio waaminifu kuingiza nchini bidhaa zisizokidhi matarajio ya matumizi katika soko. Zipo bidhaa bandia, zipo bidhaa duni na zipo bidhaa hatarishi kwa matumizi ya binadamu.

Tumesikia matukio ya ajali za moto kutokana na vifaa vya umeme bandia. Tumesikia matukio ya wananchi kupoteza maisha baada ya kutumia dawa na vipodozi hatarishi.  Aidha, ajali za vyombo mbalimbali vya moto zimehusishwa na matumizi ya vipuri bandia katika vyombo hivyo. 

Udhibiti wa soko unaofanywa na vyombo vyetu vya kudhibiti bidhaa unalenga kuwakinga walaji dhidi ya vitendo potofu katika biashara vinavyolenga kuwahadaa walaji. Hii itawawezesha wazalishaji wa bidhaa halisi kupata soko la bidhaa zao na kuifanya Tanzania nchi inayovutia wawekezaji.

Ndugu Wanasemina

Tumewaita hapa leo ili tuweze kubadilishana mawazo na kuelimishana masuala ya msingi yatakayotuwezesha kufanya biashara zetu kwa njia ambazo ni endelevu na kwa wadhibiti na wasimamizi wa soko kutekeleza majukumu yao kwa namna ambayo inazingatia uelimishaji na uwezeshaji.

Ndugu Wanasemina

Ili kujenga mahusiano mazuri baina ya vyombo vya Serikali vinavyohusika na udhibiti wa bidhaa na usimamizi wa soko, wazalishaji na wafanyabiashara tunahitaji kufanya kazi kwa pamoja ili kuleta ustawi wa biashara zetu na wananchi tunaowauzia bidhaa hizo. 

Wadau wote wafahamu kwamba madhumuni ya Serikali katika kusimamia uchumi wa soko si kukataza biashara bali kutaka ifanyike kwa kuzingatia sheria na misingi ya ushindani. Hivyo, washindani wanatakiwa kushindana na si kula njama za kukwepa kushindana sokoni.

Washindani watumie fursa iliyopo kutanzua migogoro inayohusu ushindani baina yao kwa kutumia vyombo husika kama vile Tume ya Ushindani na Baraza la Ushindani.

Aidha, Tume ya Ushindani pamoja na vyombo vingine vya Udhibiti, vitekeleze majukumu yao kwa kuongeza zaidi utoaji wa elimu kwa wafanyabiashara na kuwaelekeza zaidi kuhusu yawapasayo kutenda ili kuepuka ukiukwaji wa sheria mara kwa mara.

Ndugu wanasemina

Mwisho kabisa nivitake vyombo hivi vya udhibiti na usimamizi wa soko kuongeza utendaji kazi kwa ushirikiano wa karibu, kusisimaia kikamilifu

na kutoa huduma stahiki na kwa wakati.  Tanzania si Jalala, na kamwe haiwezi kuwa soko la bidhaa bandia kwa gharama ya uhai na maisha  ya Watanzania.  Vile vile napenda  kuwasisitiza kuepuka  rushwa na njama zozote za baadhi ya wafanyabiashara walafi wanaopenda kutumia mbinu chafu ili kuua viwanda na biashara   za wenzao  ili wabaki peke yao, na hivyo kuwalazimisha walaji kutumia bidhaa zao pekee.  Mahali pasipo na ushindani wa haki, hata viwango hushuka na bei huwa si za haki. (kiambatisho Na (1) - hatua zilizochukuliwa 2016/17.

Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji  haitasita kuchukua hatua stahiki  kwa wote watakaojihusisha na mwenendo huo.

Ndugu wanasemina,

Nafahamu kuwa Tume ya Ushindani wana makubaliano rasmi na Shirika la Viwango kuendesha kaguzi za pamoja. Vile vile Taasisi zote zinazohusika na masuala ya bandari zimeanza kufanya kazi kwa muda wa saa ishirini na nne (24). Juhudi hizi kwa pamoja zitaifanya Tanzania kwa kiwango kikubwa kuwa nchi ya kivutio cha uwekezaji kwa viwanda na sekta nyingine mbalimbali.  Hivyo, nawaomba washiriki wa semina hii muwe wasikivu na wadadisi ili kuchangia ipasavyo ukuaji wa uchumi wa viwanda katika nchi yetu.

Ndugu wanasemina, Baada ya kusema maneno haya machache, sasa natamka kuwa semina hii ya “umuhimu wa sheria ya ushindani katika uchumi wa viwanda Tanzania” imefunguliwa rasmi.

Niwakumbushe kauli Mbiu yetu "TANZANIA YA SASA TUNAJENGA VIWANDA"


Mh. Mhandisi Stella M. Manyanya, (MB)

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI

Tuesday 5 December 2017

FCC Yaadhimisha Siku ya Ushindani Desemba 5, 2017

Dar es Salaam, Desemba 6, 2017. Tume ya Ushindani nchini Tanzania imeadhimisha Siku ya Ushindani Duniani kwa kutoa mafunzo kwa wadau wa vyombo vya udhibiti na wawakilishi wa vyama vya wafanyabiashara.

Mafunzo hayo yalifanyika tarehe 5 Desemba, 2017 katika ukumbi wa GEPF, eneo la Victoria na Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Mhandisi Stella Manyanya (MB), alikuwa Mgeni Rasmi katika maadhimisho hayo.

Akifungua Rasmi maadhimisho hayo, Mhe. Naibu Waziri Manyanya aliwataka Wafanyabiashara kuepuka kuigeuza Tanzania jalala la bidhaa bandia. Aidha aliwaonya watendaji wa Serikali kuepukana na vishawishi vya rushwa katika kukagua bidhaa sokoni na katika maingilio ya bidhaa nchini.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani, Dk. John Kedi Mduma alimweleza Naibu Waziri kuwa maadhimisho hayo yametokana na Makubaliano ya Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa yaliyofanyika  tarehe 5 Desemba, 1980 ya kukubaliana kuhusu kanuni za kudhibiti vitendo vinavyodumaza ushindani duniani. Alibainisha kuwa nchi wanachama zinaadhimisha siku hii kuendelea kuwakumbusha watendaji katika mfumo wa biashara ulimwenguni kuzingatia misingi na kanuni za ushindani.

Mafunzo hayo yalihudhuriwa na watendaji kutoka Wakala wa Mbolea, Shirika la Viwango (TBS), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati (EWURA), Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), Chama cha Wenye Viwanda, Biashara na Kilimo (TCCIA), Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri wa Anga (TCAA), Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na wadau wengine.

Wadau hao pia waliweza kuelezea uzoefu wao katika kushajiisha ushindani katika soko katika utekelezaji wa shughuli zao. 

Sunday 22 October 2017

Makala ya "Umuhimu wa Tume ya Ushindani Katika Uchumi Wetu" Kutoka Hotuba ya Prof. Adolf Mkenda Akimtambulisha Kaimu Mkurugenzi Mkuu FCC, Dk. John Kedi Mduma na Kumshukuru Mkurugenzi Mkuu aliyemaliza Muda wake Dk. Frederick Ringo, mwishoni mwa Agosti, 2017

UMUHIMU WA TUME YA USHINDANI KATIKA UCHUMI WETU
 

Adolf F. Mkenda  
 
[Makala hii imeandikwa kutokana na dondoo za hotuba ya Katibu Mkuu wa Biashara na Uwekezaji aliyoitoa kwa watumishi wa Tume ya Ushindani mwezi wa nane mwaka huu. Mwandishi ndiye Katibu Mkuu wa Biashara na Uwekezaji kwenye Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji]. 

Leo nimekuja kuzungumza na nyie kwa sababu kuu tatu. Sababu ya kwanza, nimekuja kumtambulisha mtu ambaye Waziri amemteua kukaimu nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani, Dkt John Kedi Mduma. Utaratibu wa kumpata Mkurugenzi Mkuu unaendelea kwa kuzingatia Sheria iliyounda Tume, kwa hiyo wakati utaratibu huu unaendelea, Dkt Fredrick Ringo ambae muhula wake wa uongozi umeisha, atamkabidhi Dkt Mduma majukumu ya kuongoza Tume. Mpeni Dkt Mduma ushirikiano wote ili aweze kuendesha kazi hii vizuri katika kipindi hiki cha mpito.
 
Nimekuja pia kumpa Dkt Fredrick Ringo ahsante kwa kazi aliyoifanya kuongoza Tume kwa muhula aliotumikia kama Mkurugenzi Mkuu. Ahsante Dkt Ringo na tunakutakia mafanikio katika majukumu yako mengine utakayoendelea nayo.
 
Sababu ya tatu ya kutaka niwaone ni kuja kuwatia moyo na kuwahimiza muendelee na kazi nzuri mnayofanya na kutumia fursa hii kunena mambo machache kuhusu Tume.

Kazi za Tume ni ngumu sana na zinagusa maslahi makubwa ya watu ambao mara nyingi wana uwezo mkubwa wa kifedha na ushawishi. Mkikamata bidhaa bandia na kuziteketeza mnawatia hasara wale waliotengeneza au kuingiza bidhaa hizo hapa nchini; wanapoteza mamilioni na mabilioni ya fedha. Watu hawa hawatafurahi na watafanya kila njia kupambana na nyie, ikiwa ni pamoja na kuwapikia majungu. Mkiingilia mikakati ya makampuni ambayo yanataka kutumia hila ili yahodhi soko na kuumiza walaji na watu wadogo wanaozalisha malighafi mnaharibu ndoto za utajiri za makampuni haya. Hila za kujenga umiliki wa kuhodhi soko, yaani monopoly power, zinafanywa na watu ambao wana nguvu za kiuchumi na hata kisiasa kwa hiyo kupambana nao ni lazima kujifunga kibwebwe kweli kweli.
Lengo lenu jema na la kisheria la kuthibiti nyendo zisizo za ushindani wa haki linawalemea wale ambao wangependa uchumi wetu uendeshwe kwa ubabe wa mwenye nguvu mpishe, kwa kutumua the law of the jungle.  Wababe hawa siku zote watapambana na nyie kwa kila namna watakavyoweza.

Napenda kuwahakikishia kwamba Serikali iko pamoja na nyie na itasimama kidete kuhakikisha mnatekeleza majukumu yenu kwa mujibu wa sheria bila kutetereka. Chapeni kazi! Tutawalinda na kuwatetea kwa kazi mnazozifanya mradi tu mnafuata sheria, weledi na uadilifu.
 
Nawahakikishia pia kwamba tunajua sheria ni msemeno, na sheria haijali mkubwa wala mdogo, inajali tu haki. Serikali haitawaingilieni katika kutekeleza majukumu yenu kwa mujibu wa sheria na msikubali kuingiliwa na mtu yeyote. Tukianza kuwaingilia katika utendaji wenu, tutaharibu kabisa dhana nzima ya uchumi huria unaoongozwa kwa sheria na kanuni. Tukienda huko tutaacha kujenga uchumi ambao ni rule based na kujenga uchumi wa deal making. Lakini nyote mmemsikia Rais wetu akisisitiza vita dhidi ya rushwa, dhidi ya wapiga dili. Hatutakubali kujenga uchumi wa wapiga dili, tunajenga uchumi huria unaoendeshwa kwa mujibu wa sheria na kanuni.
Na ni vyema mkajua kwamba zama hizi, kuliko zama zilizopita, jukumu la mamlaka za usimamizi na udhibiti ni kubwa na muhimu zaidi. Kwanza, ni kwa sababu tumeamua kujenga uchumi wa soko huria. Kwa kujenga uchumi wa soko huria tunaachia uhuru wa watu kuzalisha na kuuza bidhaa zao bila kupangiwa na Serikali au mamlaka nyingine yeyote. Uhuru ni haki ya binadamu, kwa hiyo ujenzi wa soko huria ni hatua nyingine ya kupanua uhuru wa binadamu. Haki hii haihitaji sababu nyingine yeyote kuitetea, kwani, kama alivyosema Mwalimu Nyerere kupitia Mwongozo wa TANU wa Mwaka 1971, kwa wanadamu, “ kitendo chochote kinachowapa uwezo zaidi wa kuamua mambo yao wenyewe, ni kitendo cha maendeleo, japo kama hakiwaongezei afya wala shibe”. Kwa bahati nzuri, hatua ya kuongeza uhuru wa kiuchumi ni hatua ambayo kwa kawaida huongeza pia tija na ufanisi, na hivyo kukuza zaidi uchumi kwa ujumla. Kwa hiyo tuna sababu nzuri ya ziada ya kujenga na kuimarisha uchumi wa soko huria.

Lakini ujenzi wa soko huria sio kuachia mambo kiholela. Ni lazima bidhaa zinazozalishwa ziwe salama na zikidhi viwango. Mzalishaji na muuzaji wanao uhuru, lakini sio uhuru wa kumdanganya mlaji na kuuza bidhaa zenye madhara au ambazo hazina viwango vinavyotarajiwa na mlaji. Kadhalika, soko huria halina maana mzalishaji mmoja afanye hila kuwamaliza wazalishaji wengine ili ahodhi soko mwenyewe. Yeyote anayefanya hila za namna hii nia yake ni kuwapunja wale wanaomuuzia mali ghafi, kwa sababu mnunuzi atakuwa mmoja tu au watakuwa wachache ambao wanaweza kuunganisha mikakati yao, na pia nia inakuwa ni kuwaumiza walaji, kwani ukiondoa ushindani inakuwa rahisi kupandisha bei ya bidhaa ili kupata faida kubwa kupita kawaida. Soko huria haliruhusu uzalishaji wa hila, kwa kuingilia haki-miliki za wengine na kuzalisha bidha bandia, jambo ambalo linadhoofisha ubunifu na lina tabia ya kuzalisha bidhaa zisizokidhi viwango vya ubora na usalama. Soko huria linaendeshwa kwa kanuni, kanuni zinazo lenga kulinda haki ya walaji na wazalishaji, kuongeza ubunifu na kukuza ushindani wa haki usio na hila na ghiliba.
 
Kwa sababu sasa tumeingia katika ujenzi wa uchumi huria, kazi za mamlaka za usimamizi na udhibiti zimezidi kuwa muhimu ili kutuepusha na ujenzi wa uchumi holela. Kama nilivyosema, tunataka kujenga uchumi huria unaofuata kanuni, yaani rule-based economy, badala ya kujenga uchumi holela unaotegemea tu nani anamjua nani. Hatutaki uchumi wa deal-making, uchumi wa mwenye nguvu mpishe.
Ipo sababu kubwa ya ziada inayofanya shughuli za mamlaka za udhibiti na usimamizi, kama Tume ya Ushindani, kuwa muhimu zaidi katika zama hizi. Hii ni kwa sababu Serikali, kupitia Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano, imeamua kutenga miaka hii mitano mahsusi kwa ajili ya ujenzi wa uchumi wa viwanda. Tume ya Ushindani na mamlaka nyingine za udhibiti na usimamizi kama TBS na TFDA ni muhimu sana katika kuchochea ujenzi wa uchumi wa viwanda kwa sababu zinasimamia ubora na usalama na kujenga mazingira ya ushindani wa haki, mambo ambayo ni muhimu sana kwa wazalishaji na walaji.
Kama bidhaa za viwandani zinazozalishwa nchini hazitakidhi viwango vya ubora na usalama, wananchi wataendelea kupendelea bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ya nchi, na hivyo kudhoofisha uzalishaji wa ndani. Lazima tukumbuke kwamba kwa kuwa wanachama wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika takribani nchi ishirini na mbili zina haki ya kuingiza bidhaa zake nchini mwetu bila ukomo na bila ushuru wa forodha. Kwa hiyo hatuwezi kutegemea ushuru wa forodha kulinda bidhaa za ndani dhidi ya ushindani kutoka EAC na SADC; hatuna budi kujifunga kibwebwe na kendelea kuongeza ubora wa bidhaa zetu. Hiyo ndiyo salama yetu.
Lakini pia uzalishaji wa ndani unahitaji kutumia masoko ya nje. Jitihada za ujenzi wa uchumi wa viwanda miaka ya sitini na sabini zilishindwa kwa sababu zilijikita zaidi katika kuzalisha bidhaa kukidhi matakwa ya ndani, bila kujali sana umuhimu wa kuzingatia ushingani kwenye masoko ya nje, kwa kile kilichoitwa Import Substitution Industrial Strategy. Jitihada hizi zilitegemea sana matumizi ya ushuru wa forodha na uthibiti wa fedha za kigeni kulinda viwanda vya ndani. Mkakati huu ulishindwa kwa sababu kadhaa, na sasa hivi mkakati kama huu utashindwa zaidi kwa sababu ya kasi ya utandawazi. Ukweli ni kwamba utandawazi ni wimbi ambalo ukipigana nalo kama mkakati wa kudumu unazama, ukiogelea utaelea na unaweza kufanikiwa sana. Hapa maneno ya gwiji Shakespeare yana maana kubwa sana, kwamba:
There is a tide in the affairs of men.
Which, taken at the flood, leads on to fortune;
Omitted, all the voyage of their life
Is bound in shallows and in miseries.

 
Utandawazi umetushika, na ukishikwa shikamana. Ni muhimu tuchukulie utandawazi kama fursa ya sisi kuzalisha na kuuza kwenye masoko ya nje. Ujenzi wa uchumi wa viwanda ambao unalenga siyo tu kukidhi mahitaji ya ndani bali pia kuzalisha na kuuza kwenye masoko ya nchi za nje una faida kubwa nyingi. Kwanza unavutia wawekezaji wenye mitaji mikubwa, ambao wanajua kwamba ili kupunguza gharama za uzalishaji ni muhimu kizalisha kwa wingi mkubwa, wingi ambao soko la ndani peke yake linaweza lisimudu kununua bidhaa zote. Kwa kupunguza gharama za uzalishaji kupitia kwa wingi wa uzalishaji viwanda vyetu vitaweza kuwauzia walaji wa ndani bidhaa kwa bei ahueni na wakati huo huo kuweza kushindana kwenye soko la dunia. Zaidi ya hapo, kupanua uzalishaji wa viwanda kukidhi mahitaji ya ndani na kufukuzia masoko ya nje kutahakikisha kwamba ajira inazalishwa kwa wingi hapa nchini.
 

Hapana shaka kabisa kwamba ili kuweza kuuza bidhaa zetu kwenye soko la dunia, suala la usalama na ubora ni lazima yazingatiwe kwa kiwango cha juu. Kadhalika wazalishaji wa ndani wanaotegemea zaidi hila za kuhodhi soko la ndani kwa kudhoofisha ushindani, hawataweza kumudu ushindani kwenye soko la dunia. Kwa hiyo kazi za Tume na mamlaka nyingine za udhibiti na usimamizi ni muhimu sana katika kutuweka sawa kushindana kwenye masoko ya nje.
 
Na zaidi ya hapo, ni lazima sasa kuliko wakati wote tuzuie kabisa uingizwaji wa bidhaa zisizo na viwango na bidhaa bandia kutoka nje ya nchi. Hapa Tume inajukumu kubwa sana. Bidhaa hizi zisizo na viwango na zile bandia zinapoingia nchini zinadhoofisha sana uzalishaji wa ndani kwa kuleta ushindani usio wa haki na kudhulumu walaji.



 
Lazima tukubali kwamba bidhaa bora, salama na zisizo bandia kutoka nje zitaendelea kuingia nchini. Baadhi ya bidhaa hizo zitatoka nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki na nchi za SADC, na hivyo zitaingia nchini bila kutozwa ushuru wa forodha na bila kuwekewa ukomo. Bidhaa hizi zitaleta ushindani mkubwa kwa wazalishaji wa ndani. Lazima tukubali kuwa ushindani wa haki ni jambo jema. Ushindani wa haki humnufaisha mlaji kwa kumpa bidhaa bora na salama kwa bei ahueni. Ushindani pia hulazimisha wazalishaji wengine kuacha kubweteka na badala yake kuongeza ubunifu na ubora wa bidhaa zao. Kwa maana hiyo ushindani ni jambo bora sana. Maana ya hoja hii ni kwamba uzalishaji wa ndani hauna budi kukidhi viwango vya kimataifa, na mamlaka zetu za udhibiti na usimamizi zina kazi ya kufanikisha jambo hili. Hii ni kazi kubwa, lakini ni kazi ya lazima ili tuweze kuhimili ushindani ndani na kukabiliana na ushindani kwenye masoko ya nje.

 
Tume ya Ushindani, kwa kuondoa hila na ghiliba katika masuala ya uchumi wetu, inasaidia sana kujenga mazingira mazuri ya ushindani, mazingira ambayo yanaongeza ubunifu ambao unapunguza gharama za uzalishaji na kuongeza usalama na ubora wa bidhaa zinazozalishwa nchini. Dhima yenu hii adhimu haionekani moja kwa moja, lakini kwa hakika kazi yenu inasaidia wazalishaji wetu wasibweteke na wajue kwamba hakuna njia za panya za ghiliba. Na hii inasaidia sana kufanya wazalishaji wetu wawe washindani.

 
Kazi ya Tume ina mwelekeo wa kimahakama, na mahakama haiwezi kufanya kazi zake kwa haki bila kuwa huru. Kama nilivyosema, Serikali haitawaingilia katika majukumu yenu, badala yake itawalinda na kuwatetea mnapotekeleza majukumu yenu kwa mujibu wa sheria.

 
Walakini ningependa kuongeza mambo machache. Kuwa huru na kufuata sheria kusiwafanye mtekeleze majukumu yenu kibabe. Kazi yenu ni kusimamia sheria pasipo kutetereka, lakini kufanya hivyo kwa weledi na uadilifu. Kazi yenu sio kukomoa, kazi yenu ni kufanikisha na kuwezesha.
Serikali imeongeza nguvu katika kuboresha mazingira ya kufanya shughuli za kiuchumi nchini mwetu, na moja ya maeneo ambayo yamemulikwa sana ni kile kinachoitwa utitiri wa tozo, ada na masharti ya mamlaka mbali mbali za usimamizi na udhibiti. Kazi kubwa tayari imeshafanyika na mapendekezo yameandaliwa ya kuboresha mazingira ya kufanya shughuli za kiuchumi nchini. Zoezi hili ni endelevu, hivyo Tume, kama ilivyo kwa mamlaka nyingine, mna wajibu wa kupitia mapendekezo ambayo karibuni yatachapishwa kwa minajili ya kuona ni wapi Tume ifanye maboresho. Katika utendaji wetu wa kila siku ni budi kujitahidi kuvumbua hatua za ziada ambazo kama zitachukuliwa zitasaidia kufanya mazingira ya biashara na uchumi kuwa bora zaidi. Kwa hiyo Tume sasa inabidi, pamoja na kutekeleza majukumu yake ya kisheria, ijikite pia katika kusukuma mageuzi ya kuboresha mazingira ya biashara na uchumi, na tufanye jambo hili kama moja ya majukumu yetu.
Hata hivyo, kadiri mnavyoongeza kasi ya kutekeleza majukumu yenu ndivyo pia manung’uniko yatakavyo ongezeka. Hilo mlitegemee. Kwa kiasi kikubwa Tume itaonwa kama kero na suala hili litafikishwa kwenye medani za kisiasa mara nyingi tu. Ili mradi mnafanya kazi zenu kwa weledi na uadilifu, jambo hili halipaswi kuwatisha wala kuwakatisha tamaa.  Badala yake ongezeni nguvu katika kuuelimisha umma kuhusu umuhimu wa majukumu yenu. Tumieni kila fursa inayowezekana kuelimisha umma ili watu waelewe na kukubali majukumu yenu muhimu.
Lakini ni vyema mkajua kuwa kikipatikana kisa kimoja tu cha mtumishi wa Tume atakayekiuka maadili na weledi wa kazi yake, kisa hiki ndicho kitakachotumika na wote wenye manung’uniko kuharibu kabisa taswira ya Tume. Kisa kimoja tu kinatosha kuharibu sana kazi yenu nzuri. Kwa hakika msemo wa samaki mmoja akioza tenga lote limeoza ni muhimu sana kwa Tume katika zama hizi. Msikubali kabisa yeyote miongoni mwenu aharibu taswira ya taasisi hii muhimu. Endapo kutatokea kisa cha ukosefu wa weledi na uadilifu, chukueni hatua kali haraka sana kwa mujibu wa sheria na taratibu za utumishi. Katika hili pia Serikali itakuwa na nyie bega kwa bega. Ahsanteni.

 
LIMETOLEWA NA TUME YA USHINDANI (FCC)





 

 




Wednesday 20 September 2017

FCC Katika Channel Ten Alhamisi Septemba 21, 2017

Usikose mahojiano maalum katika Channel Ten tarehe 21 Septemba, 2017 kuanzia saa nne kamili hadi nne na nusu usiku. Maimu Mkurugenzi Mkuu, Dk. John Kedi Mduma, Kaimu Mkurugenzi wa Utetezi wa Mlaji na Udhibiti wa Bidhaa Bandia, Godfrey Gabriel, Mkuu wa Idara ya Udhibiti wa Bidhaa Bandia, Zaytun Kikula na Afisa Mkaguzi wa Bidhaa Bandia, Mike kajembe, watashiriki katika mahojiano yatakayooendeshwa na Mtangazaji Donald Mtani.
 
USIKOSE.