Wednesday 6 December 2017

Taarifa ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Dk. John Kedi Mduma katika Siku ya Ushindani Duniani Desemba 5, 2017





Hotuba ya Mgeni Rasmi, Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Mhandisi Stella Martin Manyanya (MB) akifungua Maadhimisho ya Siku ya Ushindani Duniani na Semina kwa Wadau wa Sheria ya Ushindani, GEPF House, Dar es Salaam, Desemba 5, 2017

HOTUBA YA MGENI RASMI, NAIBU  WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI, MHESHIMIWA MHANDISI STELLA MARTIN MANYANYA  (MB), KATIKA UFUNGUZI WA  SEMINA KWA WADAU WA SHERIA YA USHINDANI TAREHE 05 DESEMBA, 2017 KATIKA UKUMBI WA MIKUTANO WA GEPF
 
Mwenyekiti wa Tume ya Ushindani -  Prof. Samweli Wangwe,

Makamishna wa Tume ya Ushindani - Mr. Felix Kibodya na Mr. Fadhili  Manongi

Kaimu Mkurugenzi Mkuu Tume ya Ushindani  -Dkt. John Mduma

Menejimenti ya Tume ya Ushindani

Wawakilishi kutoka Wizara, Idara na

Taasisi za Serikali zilizopo hapa,

Viongozi wa Mashirikisho, Vyama na Jumuiya za Wazalishaji na Wafanyabiashara,

Wafanyabiashara mliohudhuria,

Wawezeshaji kutoka Tume ya Ushindani na Taasisi nyingine za Serikali,

Waandishi wa Habari,

Mabibi na Mabwana,

Itifaki Imezingatiwa

 
Habari za asubuhi,

"Awamu ya Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ni ya Uchumi wa Viwanda."

Awali ya yote napenda kuchukua fursa hii adhimu kuwakaribisha washiriki wa kikao kazi hiki kinachojumuisha Mamlaka za Udhibiti, vyama vya wafanyabiashara, wazalishaji na wanahabari.


Leo ni siku ya kipekee ulimwenguni. Ni siku ya Kimataifa ya Ushindani. Siku hii ni muhimu kwetu watendaji wa Serikali na wafanyabiashara pia. Ni siku tunayokumbushana majukumu yetu ya pamoja katika kuendesha uchumi kwa namna inayoleta na kuhakikisha ustawi endelevu katika biashara, uchumi na maslahi ya mlaji ambaye ndiye mteja.

Umuhimu wa kipekee wa siku hii unatokana na ukweli kuwa kwa sasa dunia imekuwa kama kijiji, maendeleo ya Sayansi na Teknolojia yanawezesha taarifa mbalimbali kusafiri kwa haraka kuliko miaka ya nyuma ambapo simu na barua kupitia sanduku la posta ndivyo vilivyokuwa njia kuu za upelekaji taarifa. Kukua kwa teknolojia hizi za upashanaji habari ni matokeo chanya ya kukua kwa ushindani katika sekta ya mawasiliano ulimwenguni.

Kukua kwa ushindani kumewezesha matumizi ya teknolijia za kisasa katika uzalishaji pia, kumeibua njia rahisi za uzalishaji, uuzaji na usambazaji wa bidhaa na huduma yakiwemo matumizi ya biashara mtandao.

Ndugu Wanasemina

Mabadiliko haya ya sayansi, teknolojia na utandawazi, mbali ya kuleta mafanikio yaliyoainishwa, pia yamesababisha changamoto mbalimbali katika soko. Teknolojia imerahisisha kufanyika kwa udanganyifu mkubwa katika soko unaosababishwa na wizi wa milikibunifu na alama za bidhaa ulimwenguni kote. Tanzania pia imekabiliwa na changamoto za bidhaa bandia zinazouzwa kiudanganyifu sokoni.

Ndugu Wanasemina

Sera ya Biashara ya mwaka 2003, imebainisha kuwa Tanzania imeamua kuanzisha mfumo wa kisasa wa usimamizi wa soko kwa kuweka sheria za Ushindani na Udhibiti kwa madhumuni ya kudhibiti kasoro zilizopo katika soko, hasa tabia ya ukiritimba wa soko (kuhodhi soko) ambayo huathiri na kudumaza biashara katika uchumi wa soko.

Uchumi wa soko unahitaji washiriki wengi kuweza kuingia na kufanya shughuli zao bila vikwazo na kuwepo kwa mazingira ya fursa sawa kiushindani (level playing field) ili faida zake ziweze kupatikana. Ni mfumo ambao unaongozwa na nguvu ya uhitaji na ugavi (demand and supply).

Kwa lugha nyepesi kabisa, kama una wauzaji bidhaa kama vipuri au vifaa vya umeme wachache sokoni, watakuwa wanahodhi soko hilo na wanaweza wakala njama kuweka mikakati ya kumnyonya mlaji na kufifisha ushindani baina yao. Mbinu na mikakati hiyo ni pamoja na kupanga bei, kugawana masoko kijiografia, kuficha bidhaa, kutumia vibaya nguvu za soko na kuwaondoa washindani sokoni.

Kukosekana kwa ushindani katika soko, hudumaza tija, ubunifu na ukuaji wa viwanda kwa kusababisha vizuizi vya washindani kuingia sokoni. Kwa upande mwingine, mlaji atakabiliwa na uhaba wa bidhaa.

Ndugu wanasemina

Baada ya Serikali kulegeza masharti ya biashara, kumeibuka wimbi la wafanyabiashara wasio waaminifu kuingiza nchini bidhaa zisizokidhi matarajio ya matumizi katika soko. Zipo bidhaa bandia, zipo bidhaa duni na zipo bidhaa hatarishi kwa matumizi ya binadamu.

Tumesikia matukio ya ajali za moto kutokana na vifaa vya umeme bandia. Tumesikia matukio ya wananchi kupoteza maisha baada ya kutumia dawa na vipodozi hatarishi.  Aidha, ajali za vyombo mbalimbali vya moto zimehusishwa na matumizi ya vipuri bandia katika vyombo hivyo. 

Udhibiti wa soko unaofanywa na vyombo vyetu vya kudhibiti bidhaa unalenga kuwakinga walaji dhidi ya vitendo potofu katika biashara vinavyolenga kuwahadaa walaji. Hii itawawezesha wazalishaji wa bidhaa halisi kupata soko la bidhaa zao na kuifanya Tanzania nchi inayovutia wawekezaji.

Ndugu Wanasemina

Tumewaita hapa leo ili tuweze kubadilishana mawazo na kuelimishana masuala ya msingi yatakayotuwezesha kufanya biashara zetu kwa njia ambazo ni endelevu na kwa wadhibiti na wasimamizi wa soko kutekeleza majukumu yao kwa namna ambayo inazingatia uelimishaji na uwezeshaji.

Ndugu Wanasemina

Ili kujenga mahusiano mazuri baina ya vyombo vya Serikali vinavyohusika na udhibiti wa bidhaa na usimamizi wa soko, wazalishaji na wafanyabiashara tunahitaji kufanya kazi kwa pamoja ili kuleta ustawi wa biashara zetu na wananchi tunaowauzia bidhaa hizo. 

Wadau wote wafahamu kwamba madhumuni ya Serikali katika kusimamia uchumi wa soko si kukataza biashara bali kutaka ifanyike kwa kuzingatia sheria na misingi ya ushindani. Hivyo, washindani wanatakiwa kushindana na si kula njama za kukwepa kushindana sokoni.

Washindani watumie fursa iliyopo kutanzua migogoro inayohusu ushindani baina yao kwa kutumia vyombo husika kama vile Tume ya Ushindani na Baraza la Ushindani.

Aidha, Tume ya Ushindani pamoja na vyombo vingine vya Udhibiti, vitekeleze majukumu yao kwa kuongeza zaidi utoaji wa elimu kwa wafanyabiashara na kuwaelekeza zaidi kuhusu yawapasayo kutenda ili kuepuka ukiukwaji wa sheria mara kwa mara.

Ndugu wanasemina

Mwisho kabisa nivitake vyombo hivi vya udhibiti na usimamizi wa soko kuongeza utendaji kazi kwa ushirikiano wa karibu, kusisimaia kikamilifu

na kutoa huduma stahiki na kwa wakati.  Tanzania si Jalala, na kamwe haiwezi kuwa soko la bidhaa bandia kwa gharama ya uhai na maisha  ya Watanzania.  Vile vile napenda  kuwasisitiza kuepuka  rushwa na njama zozote za baadhi ya wafanyabiashara walafi wanaopenda kutumia mbinu chafu ili kuua viwanda na biashara   za wenzao  ili wabaki peke yao, na hivyo kuwalazimisha walaji kutumia bidhaa zao pekee.  Mahali pasipo na ushindani wa haki, hata viwango hushuka na bei huwa si za haki. (kiambatisho Na (1) - hatua zilizochukuliwa 2016/17.

Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji  haitasita kuchukua hatua stahiki  kwa wote watakaojihusisha na mwenendo huo.

Ndugu wanasemina,

Nafahamu kuwa Tume ya Ushindani wana makubaliano rasmi na Shirika la Viwango kuendesha kaguzi za pamoja. Vile vile Taasisi zote zinazohusika na masuala ya bandari zimeanza kufanya kazi kwa muda wa saa ishirini na nne (24). Juhudi hizi kwa pamoja zitaifanya Tanzania kwa kiwango kikubwa kuwa nchi ya kivutio cha uwekezaji kwa viwanda na sekta nyingine mbalimbali.  Hivyo, nawaomba washiriki wa semina hii muwe wasikivu na wadadisi ili kuchangia ipasavyo ukuaji wa uchumi wa viwanda katika nchi yetu.

Ndugu wanasemina, Baada ya kusema maneno haya machache, sasa natamka kuwa semina hii ya “umuhimu wa sheria ya ushindani katika uchumi wa viwanda Tanzania” imefunguliwa rasmi.

Niwakumbushe kauli Mbiu yetu "TANZANIA YA SASA TUNAJENGA VIWANDA"


Mh. Mhandisi Stella M. Manyanya, (MB)

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI

Tuesday 5 December 2017

FCC Yaadhimisha Siku ya Ushindani Desemba 5, 2017

Dar es Salaam, Desemba 6, 2017. Tume ya Ushindani nchini Tanzania imeadhimisha Siku ya Ushindani Duniani kwa kutoa mafunzo kwa wadau wa vyombo vya udhibiti na wawakilishi wa vyama vya wafanyabiashara.

Mafunzo hayo yalifanyika tarehe 5 Desemba, 2017 katika ukumbi wa GEPF, eneo la Victoria na Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Mhandisi Stella Manyanya (MB), alikuwa Mgeni Rasmi katika maadhimisho hayo.

Akifungua Rasmi maadhimisho hayo, Mhe. Naibu Waziri Manyanya aliwataka Wafanyabiashara kuepuka kuigeuza Tanzania jalala la bidhaa bandia. Aidha aliwaonya watendaji wa Serikali kuepukana na vishawishi vya rushwa katika kukagua bidhaa sokoni na katika maingilio ya bidhaa nchini.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani, Dk. John Kedi Mduma alimweleza Naibu Waziri kuwa maadhimisho hayo yametokana na Makubaliano ya Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa yaliyofanyika  tarehe 5 Desemba, 1980 ya kukubaliana kuhusu kanuni za kudhibiti vitendo vinavyodumaza ushindani duniani. Alibainisha kuwa nchi wanachama zinaadhimisha siku hii kuendelea kuwakumbusha watendaji katika mfumo wa biashara ulimwenguni kuzingatia misingi na kanuni za ushindani.

Mafunzo hayo yalihudhuriwa na watendaji kutoka Wakala wa Mbolea, Shirika la Viwango (TBS), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati (EWURA), Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), Chama cha Wenye Viwanda, Biashara na Kilimo (TCCIA), Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri wa Anga (TCAA), Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na wadau wengine.

Wadau hao pia waliweza kuelezea uzoefu wao katika kushajiisha ushindani katika soko katika utekelezaji wa shughuli zao.