Sunday 22 October 2017

Makala ya "Umuhimu wa Tume ya Ushindani Katika Uchumi Wetu" Kutoka Hotuba ya Prof. Adolf Mkenda Akimtambulisha Kaimu Mkurugenzi Mkuu FCC, Dk. John Kedi Mduma na Kumshukuru Mkurugenzi Mkuu aliyemaliza Muda wake Dk. Frederick Ringo, mwishoni mwa Agosti, 2017

UMUHIMU WA TUME YA USHINDANI KATIKA UCHUMI WETU
 

Adolf F. Mkenda  
 
[Makala hii imeandikwa kutokana na dondoo za hotuba ya Katibu Mkuu wa Biashara na Uwekezaji aliyoitoa kwa watumishi wa Tume ya Ushindani mwezi wa nane mwaka huu. Mwandishi ndiye Katibu Mkuu wa Biashara na Uwekezaji kwenye Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji]. 

Leo nimekuja kuzungumza na nyie kwa sababu kuu tatu. Sababu ya kwanza, nimekuja kumtambulisha mtu ambaye Waziri amemteua kukaimu nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani, Dkt John Kedi Mduma. Utaratibu wa kumpata Mkurugenzi Mkuu unaendelea kwa kuzingatia Sheria iliyounda Tume, kwa hiyo wakati utaratibu huu unaendelea, Dkt Fredrick Ringo ambae muhula wake wa uongozi umeisha, atamkabidhi Dkt Mduma majukumu ya kuongoza Tume. Mpeni Dkt Mduma ushirikiano wote ili aweze kuendesha kazi hii vizuri katika kipindi hiki cha mpito.
 
Nimekuja pia kumpa Dkt Fredrick Ringo ahsante kwa kazi aliyoifanya kuongoza Tume kwa muhula aliotumikia kama Mkurugenzi Mkuu. Ahsante Dkt Ringo na tunakutakia mafanikio katika majukumu yako mengine utakayoendelea nayo.
 
Sababu ya tatu ya kutaka niwaone ni kuja kuwatia moyo na kuwahimiza muendelee na kazi nzuri mnayofanya na kutumia fursa hii kunena mambo machache kuhusu Tume.

Kazi za Tume ni ngumu sana na zinagusa maslahi makubwa ya watu ambao mara nyingi wana uwezo mkubwa wa kifedha na ushawishi. Mkikamata bidhaa bandia na kuziteketeza mnawatia hasara wale waliotengeneza au kuingiza bidhaa hizo hapa nchini; wanapoteza mamilioni na mabilioni ya fedha. Watu hawa hawatafurahi na watafanya kila njia kupambana na nyie, ikiwa ni pamoja na kuwapikia majungu. Mkiingilia mikakati ya makampuni ambayo yanataka kutumia hila ili yahodhi soko na kuumiza walaji na watu wadogo wanaozalisha malighafi mnaharibu ndoto za utajiri za makampuni haya. Hila za kujenga umiliki wa kuhodhi soko, yaani monopoly power, zinafanywa na watu ambao wana nguvu za kiuchumi na hata kisiasa kwa hiyo kupambana nao ni lazima kujifunga kibwebwe kweli kweli.
Lengo lenu jema na la kisheria la kuthibiti nyendo zisizo za ushindani wa haki linawalemea wale ambao wangependa uchumi wetu uendeshwe kwa ubabe wa mwenye nguvu mpishe, kwa kutumua the law of the jungle.  Wababe hawa siku zote watapambana na nyie kwa kila namna watakavyoweza.

Napenda kuwahakikishia kwamba Serikali iko pamoja na nyie na itasimama kidete kuhakikisha mnatekeleza majukumu yenu kwa mujibu wa sheria bila kutetereka. Chapeni kazi! Tutawalinda na kuwatetea kwa kazi mnazozifanya mradi tu mnafuata sheria, weledi na uadilifu.
 
Nawahakikishia pia kwamba tunajua sheria ni msemeno, na sheria haijali mkubwa wala mdogo, inajali tu haki. Serikali haitawaingilieni katika kutekeleza majukumu yenu kwa mujibu wa sheria na msikubali kuingiliwa na mtu yeyote. Tukianza kuwaingilia katika utendaji wenu, tutaharibu kabisa dhana nzima ya uchumi huria unaoongozwa kwa sheria na kanuni. Tukienda huko tutaacha kujenga uchumi ambao ni rule based na kujenga uchumi wa deal making. Lakini nyote mmemsikia Rais wetu akisisitiza vita dhidi ya rushwa, dhidi ya wapiga dili. Hatutakubali kujenga uchumi wa wapiga dili, tunajenga uchumi huria unaoendeshwa kwa mujibu wa sheria na kanuni.
Na ni vyema mkajua kwamba zama hizi, kuliko zama zilizopita, jukumu la mamlaka za usimamizi na udhibiti ni kubwa na muhimu zaidi. Kwanza, ni kwa sababu tumeamua kujenga uchumi wa soko huria. Kwa kujenga uchumi wa soko huria tunaachia uhuru wa watu kuzalisha na kuuza bidhaa zao bila kupangiwa na Serikali au mamlaka nyingine yeyote. Uhuru ni haki ya binadamu, kwa hiyo ujenzi wa soko huria ni hatua nyingine ya kupanua uhuru wa binadamu. Haki hii haihitaji sababu nyingine yeyote kuitetea, kwani, kama alivyosema Mwalimu Nyerere kupitia Mwongozo wa TANU wa Mwaka 1971, kwa wanadamu, “ kitendo chochote kinachowapa uwezo zaidi wa kuamua mambo yao wenyewe, ni kitendo cha maendeleo, japo kama hakiwaongezei afya wala shibe”. Kwa bahati nzuri, hatua ya kuongeza uhuru wa kiuchumi ni hatua ambayo kwa kawaida huongeza pia tija na ufanisi, na hivyo kukuza zaidi uchumi kwa ujumla. Kwa hiyo tuna sababu nzuri ya ziada ya kujenga na kuimarisha uchumi wa soko huria.

Lakini ujenzi wa soko huria sio kuachia mambo kiholela. Ni lazima bidhaa zinazozalishwa ziwe salama na zikidhi viwango. Mzalishaji na muuzaji wanao uhuru, lakini sio uhuru wa kumdanganya mlaji na kuuza bidhaa zenye madhara au ambazo hazina viwango vinavyotarajiwa na mlaji. Kadhalika, soko huria halina maana mzalishaji mmoja afanye hila kuwamaliza wazalishaji wengine ili ahodhi soko mwenyewe. Yeyote anayefanya hila za namna hii nia yake ni kuwapunja wale wanaomuuzia mali ghafi, kwa sababu mnunuzi atakuwa mmoja tu au watakuwa wachache ambao wanaweza kuunganisha mikakati yao, na pia nia inakuwa ni kuwaumiza walaji, kwani ukiondoa ushindani inakuwa rahisi kupandisha bei ya bidhaa ili kupata faida kubwa kupita kawaida. Soko huria haliruhusu uzalishaji wa hila, kwa kuingilia haki-miliki za wengine na kuzalisha bidha bandia, jambo ambalo linadhoofisha ubunifu na lina tabia ya kuzalisha bidhaa zisizokidhi viwango vya ubora na usalama. Soko huria linaendeshwa kwa kanuni, kanuni zinazo lenga kulinda haki ya walaji na wazalishaji, kuongeza ubunifu na kukuza ushindani wa haki usio na hila na ghiliba.
 
Kwa sababu sasa tumeingia katika ujenzi wa uchumi huria, kazi za mamlaka za usimamizi na udhibiti zimezidi kuwa muhimu ili kutuepusha na ujenzi wa uchumi holela. Kama nilivyosema, tunataka kujenga uchumi huria unaofuata kanuni, yaani rule-based economy, badala ya kujenga uchumi holela unaotegemea tu nani anamjua nani. Hatutaki uchumi wa deal-making, uchumi wa mwenye nguvu mpishe.
Ipo sababu kubwa ya ziada inayofanya shughuli za mamlaka za udhibiti na usimamizi, kama Tume ya Ushindani, kuwa muhimu zaidi katika zama hizi. Hii ni kwa sababu Serikali, kupitia Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano, imeamua kutenga miaka hii mitano mahsusi kwa ajili ya ujenzi wa uchumi wa viwanda. Tume ya Ushindani na mamlaka nyingine za udhibiti na usimamizi kama TBS na TFDA ni muhimu sana katika kuchochea ujenzi wa uchumi wa viwanda kwa sababu zinasimamia ubora na usalama na kujenga mazingira ya ushindani wa haki, mambo ambayo ni muhimu sana kwa wazalishaji na walaji.
Kama bidhaa za viwandani zinazozalishwa nchini hazitakidhi viwango vya ubora na usalama, wananchi wataendelea kupendelea bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ya nchi, na hivyo kudhoofisha uzalishaji wa ndani. Lazima tukumbuke kwamba kwa kuwa wanachama wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika takribani nchi ishirini na mbili zina haki ya kuingiza bidhaa zake nchini mwetu bila ukomo na bila ushuru wa forodha. Kwa hiyo hatuwezi kutegemea ushuru wa forodha kulinda bidhaa za ndani dhidi ya ushindani kutoka EAC na SADC; hatuna budi kujifunga kibwebwe na kendelea kuongeza ubora wa bidhaa zetu. Hiyo ndiyo salama yetu.
Lakini pia uzalishaji wa ndani unahitaji kutumia masoko ya nje. Jitihada za ujenzi wa uchumi wa viwanda miaka ya sitini na sabini zilishindwa kwa sababu zilijikita zaidi katika kuzalisha bidhaa kukidhi matakwa ya ndani, bila kujali sana umuhimu wa kuzingatia ushingani kwenye masoko ya nje, kwa kile kilichoitwa Import Substitution Industrial Strategy. Jitihada hizi zilitegemea sana matumizi ya ushuru wa forodha na uthibiti wa fedha za kigeni kulinda viwanda vya ndani. Mkakati huu ulishindwa kwa sababu kadhaa, na sasa hivi mkakati kama huu utashindwa zaidi kwa sababu ya kasi ya utandawazi. Ukweli ni kwamba utandawazi ni wimbi ambalo ukipigana nalo kama mkakati wa kudumu unazama, ukiogelea utaelea na unaweza kufanikiwa sana. Hapa maneno ya gwiji Shakespeare yana maana kubwa sana, kwamba:
There is a tide in the affairs of men.
Which, taken at the flood, leads on to fortune;
Omitted, all the voyage of their life
Is bound in shallows and in miseries.

 
Utandawazi umetushika, na ukishikwa shikamana. Ni muhimu tuchukulie utandawazi kama fursa ya sisi kuzalisha na kuuza kwenye masoko ya nje. Ujenzi wa uchumi wa viwanda ambao unalenga siyo tu kukidhi mahitaji ya ndani bali pia kuzalisha na kuuza kwenye masoko ya nchi za nje una faida kubwa nyingi. Kwanza unavutia wawekezaji wenye mitaji mikubwa, ambao wanajua kwamba ili kupunguza gharama za uzalishaji ni muhimu kizalisha kwa wingi mkubwa, wingi ambao soko la ndani peke yake linaweza lisimudu kununua bidhaa zote. Kwa kupunguza gharama za uzalishaji kupitia kwa wingi wa uzalishaji viwanda vyetu vitaweza kuwauzia walaji wa ndani bidhaa kwa bei ahueni na wakati huo huo kuweza kushindana kwenye soko la dunia. Zaidi ya hapo, kupanua uzalishaji wa viwanda kukidhi mahitaji ya ndani na kufukuzia masoko ya nje kutahakikisha kwamba ajira inazalishwa kwa wingi hapa nchini.
 

Hapana shaka kabisa kwamba ili kuweza kuuza bidhaa zetu kwenye soko la dunia, suala la usalama na ubora ni lazima yazingatiwe kwa kiwango cha juu. Kadhalika wazalishaji wa ndani wanaotegemea zaidi hila za kuhodhi soko la ndani kwa kudhoofisha ushindani, hawataweza kumudu ushindani kwenye soko la dunia. Kwa hiyo kazi za Tume na mamlaka nyingine za udhibiti na usimamizi ni muhimu sana katika kutuweka sawa kushindana kwenye masoko ya nje.
 
Na zaidi ya hapo, ni lazima sasa kuliko wakati wote tuzuie kabisa uingizwaji wa bidhaa zisizo na viwango na bidhaa bandia kutoka nje ya nchi. Hapa Tume inajukumu kubwa sana. Bidhaa hizi zisizo na viwango na zile bandia zinapoingia nchini zinadhoofisha sana uzalishaji wa ndani kwa kuleta ushindani usio wa haki na kudhulumu walaji.



 
Lazima tukubali kwamba bidhaa bora, salama na zisizo bandia kutoka nje zitaendelea kuingia nchini. Baadhi ya bidhaa hizo zitatoka nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki na nchi za SADC, na hivyo zitaingia nchini bila kutozwa ushuru wa forodha na bila kuwekewa ukomo. Bidhaa hizi zitaleta ushindani mkubwa kwa wazalishaji wa ndani. Lazima tukubali kuwa ushindani wa haki ni jambo jema. Ushindani wa haki humnufaisha mlaji kwa kumpa bidhaa bora na salama kwa bei ahueni. Ushindani pia hulazimisha wazalishaji wengine kuacha kubweteka na badala yake kuongeza ubunifu na ubora wa bidhaa zao. Kwa maana hiyo ushindani ni jambo bora sana. Maana ya hoja hii ni kwamba uzalishaji wa ndani hauna budi kukidhi viwango vya kimataifa, na mamlaka zetu za udhibiti na usimamizi zina kazi ya kufanikisha jambo hili. Hii ni kazi kubwa, lakini ni kazi ya lazima ili tuweze kuhimili ushindani ndani na kukabiliana na ushindani kwenye masoko ya nje.

 
Tume ya Ushindani, kwa kuondoa hila na ghiliba katika masuala ya uchumi wetu, inasaidia sana kujenga mazingira mazuri ya ushindani, mazingira ambayo yanaongeza ubunifu ambao unapunguza gharama za uzalishaji na kuongeza usalama na ubora wa bidhaa zinazozalishwa nchini. Dhima yenu hii adhimu haionekani moja kwa moja, lakini kwa hakika kazi yenu inasaidia wazalishaji wetu wasibweteke na wajue kwamba hakuna njia za panya za ghiliba. Na hii inasaidia sana kufanya wazalishaji wetu wawe washindani.

 
Kazi ya Tume ina mwelekeo wa kimahakama, na mahakama haiwezi kufanya kazi zake kwa haki bila kuwa huru. Kama nilivyosema, Serikali haitawaingilia katika majukumu yenu, badala yake itawalinda na kuwatetea mnapotekeleza majukumu yenu kwa mujibu wa sheria.

 
Walakini ningependa kuongeza mambo machache. Kuwa huru na kufuata sheria kusiwafanye mtekeleze majukumu yenu kibabe. Kazi yenu ni kusimamia sheria pasipo kutetereka, lakini kufanya hivyo kwa weledi na uadilifu. Kazi yenu sio kukomoa, kazi yenu ni kufanikisha na kuwezesha.
Serikali imeongeza nguvu katika kuboresha mazingira ya kufanya shughuli za kiuchumi nchini mwetu, na moja ya maeneo ambayo yamemulikwa sana ni kile kinachoitwa utitiri wa tozo, ada na masharti ya mamlaka mbali mbali za usimamizi na udhibiti. Kazi kubwa tayari imeshafanyika na mapendekezo yameandaliwa ya kuboresha mazingira ya kufanya shughuli za kiuchumi nchini. Zoezi hili ni endelevu, hivyo Tume, kama ilivyo kwa mamlaka nyingine, mna wajibu wa kupitia mapendekezo ambayo karibuni yatachapishwa kwa minajili ya kuona ni wapi Tume ifanye maboresho. Katika utendaji wetu wa kila siku ni budi kujitahidi kuvumbua hatua za ziada ambazo kama zitachukuliwa zitasaidia kufanya mazingira ya biashara na uchumi kuwa bora zaidi. Kwa hiyo Tume sasa inabidi, pamoja na kutekeleza majukumu yake ya kisheria, ijikite pia katika kusukuma mageuzi ya kuboresha mazingira ya biashara na uchumi, na tufanye jambo hili kama moja ya majukumu yetu.
Hata hivyo, kadiri mnavyoongeza kasi ya kutekeleza majukumu yenu ndivyo pia manung’uniko yatakavyo ongezeka. Hilo mlitegemee. Kwa kiasi kikubwa Tume itaonwa kama kero na suala hili litafikishwa kwenye medani za kisiasa mara nyingi tu. Ili mradi mnafanya kazi zenu kwa weledi na uadilifu, jambo hili halipaswi kuwatisha wala kuwakatisha tamaa.  Badala yake ongezeni nguvu katika kuuelimisha umma kuhusu umuhimu wa majukumu yenu. Tumieni kila fursa inayowezekana kuelimisha umma ili watu waelewe na kukubali majukumu yenu muhimu.
Lakini ni vyema mkajua kuwa kikipatikana kisa kimoja tu cha mtumishi wa Tume atakayekiuka maadili na weledi wa kazi yake, kisa hiki ndicho kitakachotumika na wote wenye manung’uniko kuharibu kabisa taswira ya Tume. Kisa kimoja tu kinatosha kuharibu sana kazi yenu nzuri. Kwa hakika msemo wa samaki mmoja akioza tenga lote limeoza ni muhimu sana kwa Tume katika zama hizi. Msikubali kabisa yeyote miongoni mwenu aharibu taswira ya taasisi hii muhimu. Endapo kutatokea kisa cha ukosefu wa weledi na uadilifu, chukueni hatua kali haraka sana kwa mujibu wa sheria na taratibu za utumishi. Katika hili pia Serikali itakuwa na nyie bega kwa bega. Ahsanteni.

 
LIMETOLEWA NA TUME YA USHINDANI (FCC)